VIJANA WATAKIWA KUJIEPUSHA KUKAA VIJIWENI.

Na Saada Almasi – Simiyu

Vijana waishio mkoani Simiyu wametakiwa kujiepusha na kukaa vijiweni bila kazi kujadili masuala yasiyo na maslahi kwao na taifa huku wakisubiri muujiza kutoka serikalini ili kuwainua kiuchumi badala yake waunde vikundi vya uzalishaji mali vitakavyoishawishi serikali kuwapatia mikopo itakayowatoa sehemu moja kwenda nyingine.

Ushauri huo umetolewa na katibu wa mtandao wa vijana Wazalendo Tanzania TK Movement mkoa wa Simiyu Emmanuel Mpina na kusema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa la Tanzania ambalo lina fursa nyingi ambazo zikizitumika vizuri zitawanufaisha  

“Maendeleo hayana muujiza msipo jishughulisha mkaishia kukaa vijiweni kujadili masuala yasiyo na tija kwenu huku mkiilaumu serikali hamtofanikiwa,undeni vikundi vya uzalishaji serikali iwaone halafu muone kama hamto inuliwa” – amesema Mpina

Mpina ameongeza kuwa hadi sasa tayari wanavisimamia zaidi ya vukundi kumi mkoani humo ambavyo vimejikita katika uzalishaji hivyo wao kama taasisi wameviunganisha na wadau mbalimbali pamoja na serikali waliovipatia mikopo iliyoviwezesha kujiendesha na kujinyanyua.

“Vipo vikundi hadi sasa zaidi ya kumi huko Bariadi, Meatu hapa Maswa ambavyo hadi sasa tumefanikiwa kuviingiza katika mfumo wa serikali kupewa mikopo na sasa vinawasaidia, kwa sababu moja kati ya majukumu yetu ni kuwaunganisha vijana na fursa kama hizi” Ameongeza Mpina.

Hamida Juma ni mmoja wa vijana wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa juisi ambaye kupitia mtandao huo amewataka vijana wenzake kutochagua nini cha kufanya kujiingizia kipato kwani kila jitihada zina baraka zake.

“Hii kazi ninayofanya inanisaidia kulea familia yangu kwa kupata mahitaji ya Watoto wangu sioni sababu ya vijana wenzangu kukaa vijiweni kupoteza muda,kuchagua kazi halafu waanze kuilaumu serikali kwa kushindwa kuwasaidi ,naamini kila kila jitihada zina baraka zake tujitume kufanya kazi” amesema Hamida.

Mtandao wa vijana wazalendo TK Movement upo kitaifa ambao malengo yake makuu ni kuwakusanya vijana wa kitanzania kwa pamoja wakiamini katika mgawanyo sawa wa rasilimaji za nchi kwa kuwasogeza vijana karibu na fursa ili kuwainua kiuchumi’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *