VIJANA WAPATE ELIMU YA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA VVU – KATIMBA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Zainab Katimba amesema Ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wa maendeleo kuhakikisha inawafikia vijana na kutoa Elimu ya tahadhari na Udhibiti wa maambukuzi ya Virusi vya UKIMWI katika jamii.

Katimba ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa katika hafla ya uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi wa Timiza Malengo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Tunasonga na Samia kutokomeza UKIMWI, katika uwanja wa Madini wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Amesema, mradi huo unalenga kumuelimisha kijana katika kujitambua na kuweza kujilinda na changamoto zinazochochea katika kujihusisha na tabia hatarishi zinazopelekea kupata maambukizi hasa ya virusi vya UKIMWI.

Aidha, Katimba amewapongeza watendaji wote kwenye mradi huo hasa watumishi wa OR – TAMISEMI walioko kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutoka Mikoa 10 na Halmshauri 32 kusimamia mradi huo ili uendelea kuleta tija kwa maendeleo ya vijana wa Tanzania.

Kwa upande wake, mgeni Rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ushamiri wa maambukizi ya UKIMWI kwa umri wa miaka 15-49 kimepungua kutoka asilimia 4.7 kwa mwaka 2017 hadi asilimia 4.4 kwa mwaka 2023.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Godwin Mollel amesema gharama za matibabu kwa waathirika wa UKIMWI ni kubwa hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka maambukizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *