Na William Bundala, Kahama – Shinyanga
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeipongeza Halmashauri ya Ushetu kwa kufanikiwa kuwaingiza wananchi wengi kwenye mpango wa bima ya afya kutoka kaya elfu moja hadi kaya elfu kumi na mbili.
Pongezi hizo zimetolewa na leo June 16 na mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili hoja za CAG.
“Kwakweli niwapongeze sana halmashauri ya Ushetu kwa kazi kubwa mliyofanya ya kuongeza uandikishaji wa wananchi katika bima ya afya ya CHF kutoka kaya elfu moja hadi kufikia kaya elfu kumi na mbili” Amesema Mhita.

Sambama na hayo Mhita amesema kuwa hatua hii inaonyesha halmashauri imefanya kazi kubwa ya utoaji elimu katika kuhamasisha watu kujiunga katika mfuko wa CHF hali inatakoyoimarisha huduma za afya.
“Timu ya watumishi wa halmashauri na madiwani kwakweli mnafanya kazi kubwa yani katika ofisi yangu napokea kero chache sana kutoka ushetu kuliko halmashauri zingine kwakweli hali hii inaenda kuimarisha huduma za afya”

Naye mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amesema kuwa bima ya afya inasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi na familia zao na ndiyo mana ameamua kukata bima zaidi ya elfu tatu mia nne kwa makundi mbalimbali ili ziwasaidie katika matibu.
“Ugonjwa haupigi hodi hivyo bima inasaidia kupunguza gharama za matibabu,mimi nimekata bima zaidi ya elfu tatu mia nne kwa makundi ya wenyeviti wa vitongoji,Mabalozi,wenyeviti wote wa chama cha mapinduzi katika kata na jumuiya zake na nitakuwa nawalipia kila mwaka” Amesema Cherehani.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa halmashauri ya Ushetu Athuman Matindo amesema kuwa uandikishaji umepanda kutoka kwenye asilimi tano na kufikia asilimia kumi na mbili huku huduma bora zinazotolewa na kauli nzuri kwa wateja akitaja kama kishawishi kilichowavutia wananchi wengi kujiunga na bima za afya.
“Kwa upande wa halmashauri ya Ushetu uandikishaji wa bima ya afya umepanda kutoka asilimia 5 hadi asilimia 12 na siri pekee ya mafanikio haya ni utoaji bora wa huduma za afya katika vituo vyetu Pamoja na kauli nzuri kwa wateja” Ameongeza Dkt Matindo.

Sambamba na hayo Dkt.Matindo ameongeza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuongeza makusanyo ya fedha kupitia bima ya afya kutoka milioni ishirini hadi kufikia zaidi ya shilingi million mia moja.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu tumefanikiwa kukusanya fedha kutoka shilingi milioni ishirini hadi kufikia milioni mia moja kupitia bima ya afya” Ameongeza Makindo.

Awali akizungumza kwenye baraza hilo Mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu Gagi Lala Gadi amewapongeza madiwani kwa kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya katika kata zao na juhudi zilizofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo Emmanuel Cherehani.
“Hili la bima ya afya niwapongeze sana madiwani wenzangu kwa kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya na nipongeze juhudi za mbunge Cherehani kuwalipia bima viongozi wa chama na mabalozi” Amesisitiza Lala.