Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF), imemuadhibu Meneja Habari na Mawasiliano Klabu ya Yanga SC, Ally Kamwe kulipa faini ya Shilingi milioni 5 na onyo la kutofanya kosa la kimaadili ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Kamwe amepata adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia katika tuhuma ya kuchochea umma kinyume na Kanuni za Maadili ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Toleo la Mwaka 2021.

Adhabu hiyo iiliyoanza kufanya kazi Aprili 16, 2025 imetolewa na Kamati ya Maadili kupitia kikao chake cha kupitia na kutoa uamuzi wa mashauri yaliyowasilishwa.
Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ally hakuwa na hatia, baada ya Kamati kukosa ushahidi wa kutosha kwa kosa aliloshtakiwa na Sekretarieti ya TFF akituhumiwa kuchochea kinyume na Kanuni za Maadili ya Shirikisho la soka Tanzania.
