Taiwan imepigwa na matetemeko kadhaa ya ardhi saa kadhaa kati ya Jumatatu jioni na Jumanne asubuhi ya wiki hii ikiwa iekaribia wiki tatu tabgu watu 17 alipofariki kwenye tetemeko jingine la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.4 katika vipimo vya Richta.
Tetemeko la kwanza la Jumatatu jioni lenye ukubwa wa 5.5 lilishuhudiwa kwenye kaunti ya mashariki ya Hualien, ambako ni kitovu cha lile la Aprili 3, likifuatiwa na matetemeko madogo.
Tetemeko kubwa zaidi lilishuhudiwa saa kadhaa baadaye likiwa na ukubwa wa 6.3 kulingana na kituo cha hali ya hewa cha Taipei, dakika chache baada ya jingine kutokea lililokuwa na ukubwa wa 6.0 kwa vipimo vya richta. Maafisa wa kaunti ya Hualien wamesema kuwa majengo mawili yaliyoharibiwa wakati wa tetemeko la Aprili 3, sasa yameporomoka, kufuatia tetemeko la mapema Jumanne.
Kituo cha hali ya hewa kimesema kuwa matetemeko ya sasa ni mwendelezo wa lile la Aprili 3 lakini hakuna vifo vilivyoripotiwa kwenye matukio hayo ya karibuni, ingawa shule na ofisi huko Hualien zimefungwa leo Jumanne.
Tetemeko la Aprili 3 linasemekana lilikuwa na nguvu zaidi baada ya lile la vipimo vya 7.7 lililotokea miaka 25 iliyopita na kuuwa watu 2,400, pamoja na kuharibu maelfu ya majengo.