Na Saada Almasi – Simiyu.
Waislamu mkoani Simiyu wametakiwa kutilia mkazo suala la malezi kwa watoto, ili kuondokana na kutengeneza jamii isiyokuwa na maadili mema.
Hayo yamesemwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa, Sheikh Issa Kwezi alipokuwa akitoa neno katika baraza la Eid lililofanyika wilayani Bariadi na kuwataka wazazi kuangalia upya namna wanavyoishi na watoto wao kwani malezi na maadili wanayowapatia ndiyo hujenga jamii ya kesho.

“leo hii kuna wazazi ambao hawana muda wa kulea watoto wao kutokana na utafutaji na badala yake wanalelewa ,sasa huyo mtoto mafundisho anayoyapata usitegemee akikua atabadilika la hasha atabaki hivyo hivyo na hawa ndiyo wanakuja kutengeneza jamii ambayo haina maadili na ndiyo maana nasema hata tunapotaka kuwaozesha mabinti zetu chunguzeni wachumba mnao watafutia wasije kuwa tatizo katika familia zao,” amesema Sheikh Kwezi.
Aidha Kwezi amewataka vijana kuwa makini na kujiingiza katika vyama vya siasa ambavyo vinaangalia maslahi ya vyama vyao kuliko ya taifa na ambao wanatumia vijana kuvuruga amani ya nchi ambayo kuirudisha gharama yake ni kubwa.

“vijana mjitambue msikubali kuingizwa katika maandamano yatakayoleta machafuko ,tazameni nchi jirani zisizokuwa na amani athari zake ni kubwa zingatieni maslahi ya amani ya taifa lenu kwani ikitoweka kuirudidha ni gharama kubwa,” Kwezi.
Akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Simiyu ,mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga amewataka wananchi wote walio na sifa za kujiandikisha na kujihakiki katika daftari la mpiga kura kufanya hivyo pale muda utakapofika ili wapate haki yao ya kikatiba na si kuburuzwa na watu wachache ambao hawajajiandikisha na wako tayari kuvuruga amani ilhali familia zao hazipo nchini.

“tunaelekea katika uchaguzi mkuu naomba mtumie haki yenu ya kikatiba kujiandikisha na kuhakiki muda ukifika ili mchague viongozi mnaowataka msiburuzwe na watu wachache ambao wako tayari kuvuruga amani kwa maslahi yao,mtakao athirika ni nyie na watoto wenu wenzenu familia zao ziko salama hazopo nchini,” DC Simalenga.