SERIKALI YATENGA MILIONI 350 KUTIBU MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA SIMIYU.

Na Saada Almasi- Simiyu

Mtindo wa maisha na mabadiliko ya tabia nchi  yamekuwa kati ya sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza mkoani Simiyu ,mkoa ambao ni kati ya mikoa mipya nchini ambayo ilipandishwa hadhi mnamo mwaka 2012 na kuweka idadi ya mikoa 26 Tanzania bara ambao shughuli kuu za kiuchumi kwa wakazi wa hapa ni kilimo na ufugaji.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa idadi kubwa ya wakazi wa mkoa huu kupata changamoto ya kuugua magonjwa yasiyoambukiza hali iliyosababisha Serikali kutenga zaidi ya shilingi milioni 350 mkoani humo ili kukabiliana na magonjwa hayo ambayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo sambamba na tezi dume.

Jambo FM imefanya mahojiano na Mratibu wa tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Juma Muna ambaye amesema kuwa hay ani magonjwa ambao yanamuhusu mgonjwa wenyewe tofauti yay ale ambayo mtu anaweza kukuambukiza kwa kukugusa na huanza taratibu na baadaye inafikia hatua ya kushindikana kabisa kutoka mwilini

“Magonjwa haya hayaji ghafla yanaanza muda mrefu itakumbukwa janga la korona lilipoingia watu tulizuiliwa vitu vyote ambavyo vilituweka hatarini kuambukizwa lakini hay ani tofauti yanaanza taratibu katika mwili na usipowahi kupima na kutibu hugeuka tatizo ambalo utaishi nalo miaka yote”amesema dokta Muna

Tafiti mbalimbali za wizara ya afya zinaeleza kuwa kati ya watu wazima 100 nchini watu 5 kati yao wana ugonjwa wa kisukari ama shinikizo la damu na kulingana na taarifa ya shirika la afya duniani (WHO) ya mwaka 2023 imebainisha kuwa asilimia 75 ya vifo vinavyotokea duniani husababishwa na athari za magonjwa yasiyoambukiza 

“Mfumo wa Maisha wa watu kutozingatia ulaji wa makundi yote ya vyakula, kutokufanya mazoezi, kutumia sukari nyingi na kula chumvi mbichi kupita kiasi kutopata muda wa kulala usiku yaani mitandao ya kijamii tunaitumia zaidi usiku bila kuzingatia masaa nane ya kulala na zaidi ya yote kutokuwa na desturi ya kupima afya mara kwa mara ndiko hasa kunamfanya mtu unakuja kushtuka ugonjwa umeshaanza kuleta athari kubwa “ameongeza Muna

Chamba Mathayo ni mkazi wa mtaa wa Bomani wilayani Bariadi mkoani Simiyu ambaye anamuuguza dada yake mdogo ambaye anasumbuliwa na shinikizo la damu jambo ambalo linamshangaza kwani aliamini watu wazima peke yake ndiyo waathirika pekee

“Pamoja na umri wangu huu sikuwahi kufikiri kuwa haya magonjwa wanaweza kupata Watoto wadogo lakini sasa hata mtoto wa miaka saba au minne unaambiwa ana ugonjwa wa kisukari mama yangu ni mtu mzima sana hana tatizo nadhani vijana wanatakiwa kuwa makini wabadilike hizi pombe na sigara bila kula vizuri athari zake ni kubwa” amesema Chamba

Kilio kikubwa cha wakazi wa mkoa huu ni kupewa elimu juu ya masuala ya afya kwani ukiachilia mbali harakati za utafutaji bado maadili katika jamii yameporomoka kutokana na vijana kuwa na makundi ambayo yanachochea matumizi ya vilevi ambayo yamegeuka tatizo siku za usoni

Said Juma mtaalamu wa famasi anayetoa huduma ya kuuza dawa muhimu kwa binaadamu anasema kuwa asilimia 60 ya watu anaowahudumia wanakuwa wananunua dawa za magonjwa ya moyo na kisukari .

“Wapo wanaokuja hapa wakitokea hospitali na maelezo ya dawa kutoka kwa daktarin lakini wengine huja tu wanataja dawa kutokana na kutumia muda mrefu anakuwa amesha zizowea ,mie nahudumia tu ila ni kama asilimia sitini zaidi kuliko wa magonjwa mengine” amesema Said.

Bado wito unatolewa kwa jamii kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara kwani baadhi ya magonjwa kama saratani yakigundulika mapema hutibika huku msisitizo ukitolewa kwa waliobainika na magonjwa hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *