Na Gideon Gregory – Dodoma.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekamilisha tathmini ya athari zitakazojitokeza kwa miradi ambayo ilikuwa ikipata ufadhili kupitia Serikali ya Marekani ambapo maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa yanajumuisha sekta ya afya.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo Aprili 15,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakatia akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Kagera, Neema Lugangira aliyehoji Serikali imechukua hatua gani ili kupunguza makali ya mabadiliko ya Sera za nje katika masuala ya fedha za Maendeleo Kimataifa kwa Mataifa yaliyoendelea.

“Miradi mikubwa iliyokuwa inagharamiwa kupitia mshirika huyo imetengewa bajeti kupitia fedha za ndani,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na tathmini kwa maeneo mengine yanayoweza kuathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya sera hizo za nje katika masuala ya fedha kwa kuangalia na washirika wengine wa Maendeleo ambao Serikali ya Marekani imekuwa ikitoa mchango wao.

Aidha, akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri huyo kama serikali haioni haja ya kuondoa gharama zisizo za lazima ili kuokoa fedha ambazo zinaweza kuelekezwa kuokoa mianya hiyo Dkt. Nchemba amesema tiyari suala hilo wameanza kulifanyia kazi ambapo iliunda timu iliyokuwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ili kupitia sekta zote na eneo la afya ndilo lilionekana kuhitaji kuchua hatua za haraka.