Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho na uteuzi wa viongozi mbalimbali ambapo Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka hii leo Januari 17, 2025 imeeleza kuwa Dkt. John Anthony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum.
Dkt. Grace Elias Magembe yeye ameteuliwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali, ambapo Kabla ya uteuzi huu Dkt. Magembe alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, akichukua nafasi ya Prof. Tumaini Joseph Nagu ambaye uteuzi wakeumetenguliwa.
Taarifa hiyo ambayo imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa, uhamisho na uteuzi huo umeanza mara moja.