Rais wa Russia Vladimir Putin ametoa wito kwa Moscow kujenga uhusiano na serikali ya Taliban, wakati ujumbe wa Taliban ulipoitembelea Russia.
“Siku zote tumekuwa tukiamini kwamba tunahitaji kukabiliana na hali halisi Taliban ambao wako madarakani nchini Afghanistan, tunapaswa kujenga uhusiano na serikali ya Taliban,” Putin alisema katika mkutano na vyombo vya habari vya kigeni.
Putin amesema hayo wakati akizungumza kando ya mkutano wa kimataifa wa uchumi wa mjini Saint Petersburg, ambako ujumbe wa Taliban uliwasili Juni 5,2024.
Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov wiki iliyopita alisema kwamba Moscow inapanga kuwaondoa Taliban kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi yaliyopigwa marufuku karibu miaka mitatu baada ya kundi hilo kunyakua madaraka kutoka kwa serikali iliyokuwa inaungwa mkono na Marekani ambapo Taliban walitajwa kama kundi la kigaidi nchini Russia tangu mwaka 2003.