Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameongoza Sherehe ya Familia ya Polisi (Police Family Day) na kufunga mafunzo maalum ya utayari kwa Maafisa na wakaguzi wa Polisi awamu ya pili pamoja na kupokea rasmi magari manne yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga yatakayotumika kwa shughuli za doria na kazi nyingine muhimu za ulinzi na usalama.
Sherehe hizo zilifanyika katika uwanja wa Polisi Mjini Shinyanga, ambapo Macha amekagua gwaride la polisi, kutoa zawadi na vyeti kwa maafisa na wakaguzi wa polisi waliofanya vizuri katika mafunzo ya utayari, pamoja na wadau wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi, ikiwemo kampuni ya jambo group of companies ya mjini Shinyanga
Akizungumza katika sherehe hizo, Macha ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuendelea kulijali Jeshi la Polisi, akitolea mfano msaada wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.

Amesema hatua hiyo inaimarisha ufanisi wa polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao huku akisisitiza magari hayo yatunzwe na yatumike kama yalivyokusudiwa, kutumika katika majukumu yaliyokusudiwa.
Macha pia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa utayari na nidhamu wanayoonyesha, akiwataka maafisa waliopitia mafunzo ya utayari kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi yao.
Amesema mafunzo hayo yakatumike kwa manufaa ya wananchi na kuwa faraja kwao, siyo kero na kwamba askari anayekiuka maadili lazima achukuliwe hatua za kisheria.

“Niwapongeze askari wote mlioshiriki mafunzo ya utayari. Utayari huu ukaongeze utendaji kazi wenu, huo utayari usiwe kero kwa wananchi. Jeshi la Polisi ni muhimu sana na Wananchi wana imani kubwa sana na jeshi la polisi. Tuendelee kuwatumikia wananchi kwa weledi ili waone kuwa jeshi la polisi ni kimbilio lao. Na kama kuna askari polisi anakiuka maadili lazima tumtambue na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria”,amesema Macha.
Natamani kuona kila kata kuna ulinzi shirikishi, kuwe na vikundi vya kutambua watu wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu, viongozi wa serikali za mitaa wawatambue watu waliopo katika maeneo yao ili tufahamiane. Suala la ulinzi siyo la Polisi peke yao, hili jambo haliwezi kuwa la polisi tu lazima tuungane sote”,ameongeza Macha.

Kwa upande wa usalama barabarani, Macha ametoa maagizo kwa kitengo cha usalama barabarani kudhibiti tabia mbaya za baadhi ya madereva wa mabasi, na kuwataka askari polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waendesha bodaboda wanaokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na kubeba abiria wengi ‘mishikaki’ na kubeba watoto kwenye matanki ya mafuta ya pikipiki.
Aidha, Macha ameviasa vyama vya siasa kuhakikisha vinaheshimu sheria za nchi hasa wakati huu taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Ametaka shughuli za kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani na utulivu na kuepuka maandamano yasiyo na tija.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amesema kwamba Sherehe ya Familia ya Polisi inahusisha kukutanisha familia za polisi,
Amesema lengo la sherehe hizo ni kutoa motisha kwa maafisa wa polisi na familia zao, kusherehekea mafanikio ya mwaka, na kupanga mikakati ya kiutendaji kwa mwaka huu, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Mgani pia ameeleza kuwa mafunzo maalum ya utayari kwa maafisa na wakaguzi wa polisi Mkoa wa Shinyanga yalifanyika kwa awamu mbili, na kwamba lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha maafisa na wakaguzi kuwa na ujasiri, umahiri, weledi, na ukakamavu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza, hasa wakati wa uchaguzi.