Ndege mpya ya abiria (Boeing 737 max9) kutoka nchini Marekani yenye uwezo wa kubeba watu 181, mizigo tani sita na uwezo wa kuruka kwa saa 8 bila kutua imewasili nchini.
Pamoja na kupokea ndege hiyo pia serikali itakabidhi ndege mbili za mafunzo kwa Chuo cha Usafirishaji (NIT) zenye uwezo wa kubeba watu wanne kwa ajili ya mafunzo ikilenga kuongeza wataalamu wa ndani kuzihudumia ndege hizo.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akiongea na waadishi wa habari Octoba 2 2023 alisema kufikia mwaka 2025 Tanzania itakuwa na jumla ya ndege 16 jambo ambalo litaongeza wigo katika sekta ya Utalii na biashara kwa lengo la kukuza pato la Taifa.
Itakumbukwa kuwa safari hii ya mafanikio ilianza mwaka 2016 katika harakati za kulifufua Shirika la Ndege nchini (ATCL), ambapo mpaka kufikia leo tayari zipo ndege 13.
ATCL kwa sasa inahudumia vituo vya ndani 14 na vingine vya nje vikiwemo Entebe, Kenya, Burundi, Comoro, Zimbabwe, Mumbai na China.