MZOZO ENEO LA KIWANDA: CHALAMILA AFIKA WAZO HILL

Kufuatia uwepo wa mzozo wa uvamizi wa eneo la Kiwanda cha Sayuji Wazo Hill, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametembelea mahala hapo ili kujionea malalamiko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitolewa na uongozi wa kiwanda hicho.

Chalamila ametembelea Kiwandani hapo hii leo Januari 17, 2025 na kusema uvamizi wa eneo hilo umepelekea kiwanda kuwa na eneo dogo, na kuathiri mifumo ya upatikanaji wa maji toshelevu kwa matumizi ya kiwanda.

Katika kutafuta suluhu ya malalamiko hayo, Chalamila amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuitisha mkutano utakaowajumuisha wananchi wa eneo hilo, uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na uongozi wa kiwanda wiki ijayo, ili kuanza upya mazungumzo.

Aidha, amemtaka Mtendaji Mkuu DAWASA kufika mara moja katika kiwanda hicho kuketi na Menejimenti ya Kiwanda hicho, ili kuona namna bora ya kumaliza changamoto hiyo.

RC Chalamila pia amemuagiza Naibu Kamishna wa Ardhi Mkoa kwa kushirikiana na Wanasheria chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa kuunda kamati ndogo ambayo itapitia malalamiko na hukumu zilizotolewa na Mahakama juu ya eneo hilo ili kuweza kumshauri Mkuu wa Mkoa njia sahihi za kupita kwa lengo la kupunguza malalamiko kwa mwekezaji.

Amesema, Kiwanda hicho ni muhimu kwa masilahi mapana ya umma, kwa kuwa kimekuwa kikitoa fursa kubwa ya ajira, lakini pia huchangia katika pato la Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *