Bingwa mara mbili wa Olimpiki raia wa Afrika Kusini, Caster Semenya ameshinda kesi ya rufaa kwenye Mahakama ya haki za binadamu, juu ya kanuni zinazosimamia homoni za kiume (testosterone) kwa Wanariadha wa kike kwenye mashindano.
Mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu imefikia uamuzi kuwa, mwanariadha huyo alibaguliwa na vilevile hakutendewa haki kwa kunyimwa mara mbili kukata rufaa na Mahakama ya usuluhishi ya michezo, pamoja na Mahakama Kuu ya Uswizi.
Semenya (32) ana hali ya kiafya inayohusika na kuwa na homoni za kiume nyingi kuliko kawaida. Homoni hizo huongeza vitu kadhaa ikiwemo uzito wa misuli na nguvu ambazo humuongezea uwezo.
Kisheria, ili kushiriki kwenye mashindano ya wanawake, mwanariadha mwenye hali kama hiyo hutakiwa kupunguza homoni hizo kwa kutumia vidonge, sindano au upasuaji ili ziwe sawa na za mwanamke wa kawaida.
Uamuzi huo unaweza kuilazimu Mahakama ya usuluhishi ya michezo kupitia upya kanuni zake juu ya suala hili.
Bado haijajulikana kama uamuzi wa Mahakama ya haki za binadamu utamruhusu Semenya kushiriki kwenye mashindano ya Olimpiki 2024 jijini Paris.