Mtoto Julius Kazungu (10) mwenye mlemavu wa ngozi (Ualbino) mkazi wa mtaa wa Mtakuja katika mji mdogo wa Katoro wilaya na Mkoa wa Geita amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na mtu asiyejulikana hali iliyopelekea damu nyingi kuvuja kabla ya kukimbizwa hospitali ili kuokoa uhai wake.
Akizungumza na Jambo Fm nyumbani kwake, mama mzazi wa mtoto huyo Frola Nzumbi amesema tukio hilo limetokea Mei 4 mwaka huu majira ya saa moja usiku wakati mtoto huyo akiwa anarudi ndani kutoka chooni ndipo alivutwa kwa nyuma na mtu asiefahamika na kumjeruhi na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake ndipo akaanza kupiga kelele hali iliyopelekea mtu huyo kukimbia kusikojulikana na kumuacha mtoto huyo akivuja damu.
Akithibitisha kumpokea mtoto huyo katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Geita Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Thomasa Mafuru amesema mtoto huyo alifikishwa na gari la kubebea agojwa majira ya saa tano usiku Mei 4 mwaka huu na walipomfanyia uchunguzi walibaini kwamba amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani, sehemu ya mkono wa kulia pamoja na kwenye kidole cha mkono huo.
Nao baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo amesema walimuona mtoto huyo anachota maji kisha kupeleka chooni lakini wakati anarudi alishikwa mgongoni na mtu ambae hakufahamika na awali walidhani kuwa ni mtoto mwezake lakini badae wakasikia mtoto Yule kama anapigwa na ubapa wa panga na walipokimbia kwenda kumuona waliona mtu kwa mbali akikimbia na mtoto tayari alikuwa ameshajeruhiwa.
Kwa upande wake katibu wa chama cha albino wilaya ya Geita Leah Magesa amesema chama hicho kimeshtushwa kwa kiasi kikubwa na tukio hilo kwani kwa zaidi ya miaka nane matukio ya aina hiyo yalikuwa yamesahaulika na kutumia nafasi hiyo kukemea vikali matukio kama hayo kwani yamekua yakigharimu maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Safia Jongo amesema mtoto huyo alivamiwa na mtu huyo wakati alipokuwa ametumwa na mama yake nje ndipo mtu huyo akaanza kuchana na panga sehemu za kichwani, mkononi kisha panga hilo likamjeruhi kwenye kidole lakini uchunguzi wa awali umebaini tukio hilo lilikuwa limepangwa
One response to “Mtoto Mwenye Ualbino Ajeruhiwa Kichwani, Mkono na Kidole-Geita”
Mungu Mwenyezi amjalie kupona mapema.