Hali ya kisiasa ndani ya Chama Kikuu cha Upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inazidi kuwa tete baada ya leo wanachama wake zaidi ya 100 kutoka kwenye majimbo 11 mkoani Tabora, wakiongozwa na Mwenyekiti wao James Kabegele, kutangaza kujiondoa kwenye chama hicho.
Wakizungumza sababu za wao kujiondoa kwenye chama hicho kilichogubikwa na mgogoro mkubwa unaokimbiza makada wake, wamesema ni kutokana na kudharauliwa pamoja na msimamo wa chama chao kususia kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu mwezi Oktoba.

Kabelege amesema baada ya kuondoka Chadema, watatoa msimamo wao na mwelekeo wao kisiasa pamoja na maeneo wanayoelekea ili kuendelea na harakati zao za kisiasa.
Kumekuwa na mpasuko mkubwa ndani ya Chadema hali inayosababisha viongozi na makada wake wengi kuamua kukihama chama hicho nchini.
Wengi wanaoamua kuondoka Chadema wanautaja uongozi mpya wa chama hicho unaoongozwa na Mwenyekiti wake Tundu Lissu kuwagawa makada wake pamoja na kudharau ushauri kama mwendelezo wa kuangamiza kambi ya mgombea mwenzake Freeman Mbowe.