Jumla ya shilingi millioni 177.3 zimekusanywa katika harambee ya kuichangia klabu ya soka ya Pamba Jiji FC inayoshiriki ligi ya NBC Championship.
Harambee hiyo imefanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Mwanza Hotel ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ambapo fedha hizo zimetoka kwa watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi, ikiwa na lengo la kuipa nguvu klabu hiyo katika harakati zake za kurejea ligi kuu.
Fedha hizo zilizotokana na harambee ni pamoja na michango taslimu ambayo ni zaidi ya Shilingi milioni 28 huku ahadi ikiwa ni zaidi ya Shilingi milioni 100.
Pamba Jiji FC inayodhaminiwa na Jambo Food Products kupitia kinywaji chake cha Xtreme Energy Drink kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimo wa ligi ya Championship ikiwa na alama 44 nyuma ya Biashara United FC yenye alama 46 na Kengold yenye alama 47.