MD TWANGE, DC MTATIRO WAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 jamii inatumia nishati safi ya kupikia, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kuhamasisha matumizi ya vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme kwa ufanisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, kifaa hicho  cha kupikia aina ya pressure cooker kinachotumia umeme mdogo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuelimisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika leo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Twange amesema kuwa sekta ya nishati kwa sasa haijajikita tu katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, bali pia ina jukumu la kuhamasisha matumizi bora ya nishati hiyo majumbani.

“Tunataka wananchi waelewe kuwa matumizi ya nishati safi ni salama kwa afya, ni rafiki wa mazingira, na yanapunguza gharama kwa muda mrefu. Hili ni moja ya majukumu mapya ya TANESCO katika kulinda mazingira na kusaidia juhudi za kitaifa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Twange.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amelishukuru shirika hilo kwa mchango huo na kuahidi kuwa serikali ya wilaya kupitia ofisi yake itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara, ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuachana na nishati chafu.

“Nitahakikisha jamii ya Shinyanga inapata elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya nishati safi, na tutafanya hivyo kupitia mikutano ya vijiji na kata. Tunahitaji mabadiliko ya kimtazamo ili kuokoa mazingira yetu na afya za wananchi,” Amesema  Mtatiro.

Mkurugenzi huyo wa TANESCO yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa katika mkoa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *