Matumizi ya Silaha Duniani Yaongezeka Kwa asilimia 7

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani na usalama SIPRI kutoka Sweden, imesema matumizi ya kijeshi kote duniani yameongezeka kwa asilimia 7, ikiwa ni sawa na dola trilioni 2.43 kwa mwaka 2023 ongezeko ambalo ni kubwa tangu kuripotiwa kwa ongezeko la mwaka 2009 na ripoto imeyataja mataifa ya Marekani,China na Urusi kuwa na matumizi makubwa ya Kijeshi kwa mwaka 2023.

Mtafiti Mkuu katika mpango wa uangalizi wa matumizi ya kijeshi na utengenezaji wa silaha wa SIPRI Nan Tian amesema ongezako limetokana na kudorora kwa amani na usalama wa dunia na kudokeza kwamba mataifa yameweka mbele nguvu za kijeshi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama wa dunia.

SIPRI imesema Urusi kwa mfano, imeongeza matumizi yake kwa asilimia 24 ambayo ni sawa na dola bilioni 109, Ukraine nayo imeongeza matumizi hayo ya kijeshi kwa asilimia 51, sawa na dola bilioni 65 na kupokea angalau dola bilioni 35 za msaada wa kijeshi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi.

SIPRI imeongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO zimetumia takriban asilimia 55 ya matumizi ya kijeshi duniani. Mtafiti mwengine wa SIPRI, Lorenzo Scarazzato, amesema miaka miwili ya vita vya Urusi nchini Ukraine imebadilisha kabisa muonekano wa usalama na kutoa kitisho zaidi cha usalama badala ya amani na uthabiti duniani.

Watafiti wa taasisi hiyo wamesema wanakadiria katika utafiti watakaoufanya wa mwaka 2024 matumizi ya kijeshi huenda yakaongezeka zaidi kufuatia shambulizi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas, katika Ukanda wa Gaza na wasiwasi uliopo katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati ya mzozo kutanuka pia, umesababisha matumizi hayo kuongeza kwa kiasi kikubwa kuwahi kushuhudiwa ndani ya miaka 10 iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *