Serikali Nchini, imezitaka nchi za Malawi na Afrika Kusini kufungua masoko yao kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania hadi kupikia Jumatanonijayo Aprili 23, 2025, la sivyo itachukua hatua ya kuzuia bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo kuingia nchini pamoja na kupita katika ardhi ya Tanzania kuelekea kwenye masoko mengine.
Onyo hilo, limetolewa hii leo Aprili 17, 2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akieleza kuwa Tanzania imechoshwa na vikwazo visivyo na maelezo vinavyowekwa na baadhi ya nchi jirani dhidi ya mazao ya Watanzania.
“Tupokee taarifa kuwa nchi ya Malawi imezuia mazao mbalimbali kuingia nchini kwao. Mazao hayo ni pamoja na unga, mchele, tangawizi, ndizi na hata mahindi, jambo ambalo limesababisha wafanyabiashara wetu wa Kitanzania kushindwa kuingiza mizigo katika nchi hiyo,” aliandika Bashe.

Aidha ameongeza kuwa, “kwa mara ya mwisho, tunaendelea na jitihada za mawasiliano na Serikali za ‘South Africa’ na Malawi hadi kufikia Jumatano ijayo. Tukikosa mrejesho, Wizara ya Kilimo itazuia mazao yote ya kilimo na bidhaa zote kutoka South Africa na Malawi.”
Chapisho la Bashe limeeleza zaidi kuwa, Tanzania haitaruhusu tena mazao kutoka Malawi au Afrika Kusini kutumia ardhi ya Tanzania kwenda katika bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine, na kwamba hatua kama hiyo iliwahi kuchukuliwa mwaka jana hadi mataifa hayo yalipofungua masoko yao.
“Tanzania itasitisha usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi kama sehemu ya hatua za kujibu vikwazo hivyo, akitoa notisi kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kuwa wasipakie mizigo yoyote kuelekea Malawi kuanzia Jumatano wiki ijayo, iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya msimamo kutoka nchi hizo,” ameonya Bashe.