Majaliwa aagiza kukabidhiwa Taarifa ya Udhibiti Uvuvi Haramu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza taarifa maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya makadirio  bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka fedha 2024/2025.

Ametoa agizo hilo leo Jumapili, Aprili 21, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa boti maalum kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari hapa nchini iliyofanyika bandarini jijini Dar es Salaam.

Aidha ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mipango ya maendeleo ambayo imechangia dola za Marekani 500,000 kwenye ununuzi wa boti hiyo na vilevile, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuchangia dola za Marekani 400,000 kwenye mradi huo.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga alieleza kuwa ununuzi wa boti hiyo ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari na maziwa makuu unaotekelezwa na Serikali.

Amesema mapambano hayo yatahusisha kuimarisha juhudi za kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya na utoroshwaji wa nyara za Serikali na akieleza sifa za boti hiyo ya doria iliyopewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB Sailfish) amesema ni boti ni mpya, ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa majukumu ya doria.

Ameongeza kwamba uwepo wa boti hiyo utaleta mageuzi makubwa kwenye ulinzi na usalama wa baharini kwani itawezesha kufanya doria na kaguzi kwenye maji ya Tanzania na kufanya utafutaji na uokozi pindi zikitokea ajali baharini na kuimarisha ulinzi kwenye pwani ya Tanzania kwa kuwa imewekewa mitambo maalum ya silaha pamoja na mtambo maalum wa kuzima moto.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano hayo na kueleza umuhimu wa mradi kuwa utaimarisha uwezo wa Tanzania wa kuzuia shughuli haramu ndani ya bahari ya Tanzania.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameishukuru Serikali kwa kupatikana kwa boti ya doria kwenye bahari na maziwa makuu kwa sababu itatatua changamoto ya uhalifu na kuishukuru serikali kwa kupambana na milipuko baharini pamoja na kuwakabili wahusika wa vilipuzi ambapo hadi sasa watuhumiwa wapatao 24 wamekamatwa,Kati ya hao, 13 ni wasambazaji wa vilipuzi, 10 ni wavuvi na mmoja ni mfadhili wao.

Akitoa taarifa kuhusu ufanisi wa boti hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema boti hiyo ina uwezo kukimbia kwa kasi ya km. 47 kwa saa (nautical miles 25), inaweza kubeba wahalifu 20 kwa pamoja, inaweza kutumika kubebea wagonjwa (ambulance), kuzima moto na kwenye shughuli za uokoaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *