Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga na kusababisha madhara makubwa ikiwemo kifo cha mtu mmoja wananchi wameiomba serikali kumsimamia mkandarasi anayejenga Barabara katika manispaa hiyo kupitia mradi wa TACTICS ili atekeleze kwa wakati kwani mitalo mingi aliyochimba ndio imesababisha mafuriko hayo.
Wakizungumza na Jambo Fm kwa nyakati tofauti wananchi hao wmesema kuwa maji mengi yamepita sehemu isiyo rasmi na kuingia kwenye nyumba za watu kwakuwa njia za maji zimefungwa na vifusi kufuatia ujenzi wa Barabara za manispaa.
“Haya maji yana njia yake miaka yote sasa huyu mkandarasi angekuwa anajenga kipande kimoja kimoja sasa yeye kachimbua kila kona na vifusi kaweka kwenye njia za maji ndo madhara haya mnayoyaona,Serikali imsimamie ujenzi ukamilike mbona anasua sua hivi” Amesema mmoja wa wanachi wa mtaa wa Majengo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Majengo Zacharia Miligo amesema kuwa katika mtaa wake maji yaliingia ndani katika ya nyumba za watu na Barabara moja ya bondeni imekatika na kusombwa na maji hali inayosababisha kutopitika kabisa.
“Katika mtaa wangu maji yaliingia kwenye makazi ya watu na kuharibu thamani za watu kwa kiasi kikubwa na kuna sehemu moja inaitwa bondeni Barabara imekatika na kusombwa na maji hivyo inahitaji kurekebishwa ili maji yapite kwenye njia yake” Amesema Miligo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio la kifo la binti huyo ambaye hajajulikana jina na mahali anapoishi Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema binti huyo alisomwa na maji ya mvua baada ya kuzama kwenye mtaro uliokuwa umejaa maji akijaribu kuvuka na kuwataka wananchi kuwa waangalifu kipindi hiki cha Mvua.

“Ni kweli tukio hilo lipo limetokea April 6 maeneo ya Kahama mjini binti alisombwa na maji akijaribu kuvuka kwenye mtaro uliojaa maji,niwaombe wananchi kuwa waangalifu kipindi hiki cha mvua ambacho zinatajwa kunyesha kwa wingi” Amesisitiza Mgomi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita Amemuagiza meneja wa TARURA Kahama kuhakikisha anashirikiana na mkandarasi anayejenga Barabara kupitia mradi wa TACTICS kuzibua mitaro ili kuzuia mafuriko katika kipindi hiki cha Mvua zinazoendelea kunyesha.
“Zuieni ujenzi holela wa makazi husani wanaojenga Katikati ya njia za maji ili kuepusha madhara zaidi,Meneja TARURA shirikiana na mkandarasi anayetekeleza mradi huu kuzibua mitaro ili kuzuia mafuriko katika mitaa” Amesema Mhita,