Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki, Doreen Sinare amesema Muziki wa singeli umeendelea kukua kwa kasi Nchini na kupendwa zaidi nje ya nje ya mipaka ya Tanzania na kwamba hata Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alieleza namna alivyoshuhudia wazungu wakiufurahia.
Sinare ameyasema hayo hii leo Machi 21, 2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya miaka minne ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan
Amesema, “katika kipindi hiki, COSOTA imetoa elimu kwa Wasanii, watayarishaji, wafanyabiasha na wadau wa Singeli kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uswazi Got Talent na Kandoro Baba Entertainment chini ya Meneja Kandoro kuwaeleza umuhimu wa usajili wa kazi zao na faida za kusajili ambapo takribani wasanii 20 wa Muziki wa Singeli wamesajili kazi zao COSOTA.”

“Pia wamenufaika na mgao wa mirabaha kwa mwaka 2022 na mwaka 2023 na nimategemeo yetu kuwa watanufaika Zaidi kutokana na kupendwa na kushiriki katika biashara ya muziki wa singeli ndani na nje ya nchi,” aliongeza Sinare.
Hata hivyo, amesema Serikali kupitia Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ilihaidi kuimarisha usimamizi wa hakimiliki na kuhakikisha Wasanii wananufaika zaidi na kazi zao pamoja na kupata mirabaha na ametekeleza.

“Kati ya mambo yaliyofanyika ni pamoja na marekebisho katika Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 yaliyofanyika mwaka 2022 na 2023 kupitia Sheria za Fedha za mwaka 2022 na 2023,” amesema.
Sinare amesema mabadiliko hayo makubwa yalianzisha chanzo kipya cha mapato cha tozo ya hakimiliki (copyright levy), ambapo vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi kazi za sanaa na fasihi hutozwa asilimia moja nukta tano (1.5%) kila vinapoingia, kuzalishwa au kuundwa hapa nchini.