Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kufuatia tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imeeleza kuwa, tukio hilo limetokea Aprili 9, 2025, katika mtaa wa Soko Kuu, Wilaya ya Mbinga, ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chilya amesema Lissu alikamatwa alitoa kauli zinazoweza kuashiria kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu ujao.

Amesema, uchunguzi kuhusu tuhuma hizo ulikuwa unaendelea kwa muda kabla ya kuchukuliwa hatua ya kumkamata na alihamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi na maafisa wa upelelezi.
Kamanda Chilya ameongeza kuwa, uchunguzi unafanyika, ili kubaini kama kuna msingi wa kisheria wa kumfikisha mahakamani.

Aidha, ameonya vyama vyote vya siasa na viongozi wao kuwa makini na kauli wanazotoa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani wanafuatilia kwa karibu matamshi ya kisiasa yanayotolewa kwenye mikutano, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Amewataka wanasiasa kujiepusha na lugha ya kukashifu vyombo vya dola au serikali kwa ujumla, kwani kufanya hivyo kunaweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuathiri usalama wa taifa. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na sheria.