KUWASA YAPATA CHANZO KIPYA CHA MAJI KAHAMA

Serikali Wilayani Kahama imeiopongea Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) kwa kuanzisha chanzo mbadala cha upatikanaji wa maji kuliko kutegemea chanzo kimoja cha ziwa Victoria.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita katika kikao cha kupokea ripoti ya utekelezaji wa mtandao wa maji wilayani Kahama.

Mhita amesema, Manispaa ya Kahama inakuwa kwa kasi hivyo kutegemea chanzo kimoja cha maji cha ziwa Victoria ni kukwamisha shughuli za maendeleo hivyo kuanzishwa kwa chanzo hiko tutakuwa na uhakika wa maji marakwa mara.

“Niwapongeze sana KUWASA kwa kuja na wazo hili,Kahama ni mji unaokuwa kwa kasi na ni lango kubwa la nchi za Africa mashariki inahitaji upatikanaji wa maji muda wote” Alisema Mhita.

Sambamba na hayo Mhita ametoa rai kwa wananchi wa Kahama kuacha kuharibu miundo mbinu ya maji na kwamba msako mkali unaanzishwa kwaajili ya kuwabaini waharibifu na kuwachukulia hatua.

“Serikali inafanya juhudi kubwa kuleta maendeleo kwa wananchi,Wana Kahama nawaomba muwe wazalendo kulinda miundo mbinu ya maji na kuitunza nataka niseme tunaanza msako mkali kuwabaini waharibifu na kuwachukulia hatua,” ameongezea Mhita.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Allen Marwa ameishukuru serikali kwa kutoa pesa nyingi kupitia Wizara ya Fedha hali iliyosadia kupanua huduma ya maji kwa wananchi.

“Kwakweli tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutupatia fedha za kutosha kwaajili ya kutekeleza miradi ya maji,Hakika tunaende kupanua miradi ya maji kwa kiasi kikubwa na hadi kufikia hatua ya mwisho tutaweza kuwafikia wanachi kwa asilimia 96,” alisema Marwa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Chujio la maji Mwendakulima, Mkurugenzi wa Usambazaji (KUWASA), Magige Marwa amesema chanzo hicho kipya cha Maji kitakuwa na uwezo wa kuchuja Lita milioni 10 na kitatoa huduma kwa muda wa miezi mitatu mfululizo na kuondoa Changamoto ya upatikanaji wa maji kwa manispaa ya Kahama.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, chujio la maji ambalo tunalijenga kwenye kongani ya Buzwagi itakuwa na uwezo wa kuchuja Lita milioni 10 kwa siku na ujazo wake utaweza kutumika kwa muda wa miezi mitatu mfululizo,“ alisema Magige.

Ujenzi wa Chujio la maji Mwendakulima unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni tatu na milioni miatatu unatarajia kukamilika mwezi wa pili mwakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *