By Frank Aman – Geita.
Jeshi la Polisi Mkoani Geita limemfikisha katika Mahakama ya Mwanzo ya Nyankumbu wilayani Geita mtuhumiwa Alfred Joseph (25) baada ya kukamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za wizi wa fedha shilingi milioni 8 alizomwibia mwajiri wake Gabriel Albert, mfanyabiashara ya huduma za kifedha.
Akisoma shtaka hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Bw. Ally Mgomba amesema mtuhumiwa alifanya tukio hilo Machi 28, 2025 majira ya saa 12 alfajiri kinyume na kifungu 258 na 265 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 (iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022).

“Baada ya mshtakiwa kuiba fedha kiasi tajwa alitoroka na kwenda kujificha Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga. Na uchunguzi wa tukio hili ulipofanyika sambamba na kumkamata mtuhumiwa ambaye amekiri kuiba na kuzitumia pesa hizo alizoiba kumlipia mahari mke wake (jina linahifadhiwa) kiasi cha milioni 2, kununua pikipiki MC.236 DXP milioni 2, kununua samani mbalimbali za ndani na kulipia chumba cha kuishi,” amesema.
Jeshi la Polisi Mkoani Geita linawataka wafanyabiashara kuhakikisha usalama wa mali zao na kuweka mifumo ya ulinzi inayozuia watumishi wao kushawishika kujiingiza kwenye uhalifu.
One response to “JOSEPH AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA WIZI WA MIL. 8 ZA MWAJIRI WAKE”
Duh huyu jamaa hatari