Vumilia Kasomelo mkazi wa kisiwa cha Kome katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia kumjeruhi mwanamke mwenzie kwa kummwagia maji ya moto katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Morice Mtoi akisoma mashtaka dhidi ya mshtakiwa (Vumilia) amesema tukio hilo lilitokea tarehe 26 Agosti 2023 majira ya saa 21:00 Usiku ambapo Vumilia alitenda kosa hilo la kummwagia maji ya moto Mariam Paulo (36) katika kijiji cha Lugata, tarafa ya Buchosa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kosa ambalo ni kinyume na kifungu namba 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2022.
Hata hivyo mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo kutokana na hasira baada ya kuoneshwa na watu waliokuwa kwenye msiba wa Baba mkwe wao kuwa Mariam ni mke mwenzie kwa mume wao aitwaye Ndagabwene Evarist (38).
Baada ya kupewa hukumu hiyo mshtakiwa (Vumilia) aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu hiyo ila Mahakama imemhukumu kutumikia kifungu hicho cha miaka mitatu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
