Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeutaarufu Umma kuwa haijafanya mazungumzo wala kutoa maelekezo yoyote ya kupewa leseni au kuruhusiwa kwa kampuni ya Leo Beneath London (LBL), kama ambavyo taarifa mbalimbali zinavyosambaa mitandaoni.
Taarifa iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba imeeleza kuwa, hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa kampuni ya LBL kwa kujihusisha na ulaghai ikiwemo kupokea amana, kutoa riba na kufanya uhaulishaji wa fedha
bila leseni ya Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha, taarifa hiyo imewatahadharisha Wananchi kuepuka kujihusisha na Taasisi, Kampuni au mtu binafsi ambaye anatoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni ya Benki Kuu, au Wasimamizi
wengine wa huduma za fedha.

“Benki Kuu inawaonya watu na taasisi ambazo zinatumia jina la Benki Kuu kuuhadaa Umma katika vitendo vyao vya kihalifu, kuacha kufanya hivyo vinginevyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao,” ilieleza taarifa hiyo.
Benki Kuu pia imewahimiza Wananchi wanaotaka kupata huduma za kifedha kutumia taasisi zenye leseni ambazo orodha yake inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu (www.bot.go.tz) au wasimamizi wengine wa sekta ya fedha nchini.
Aidha, Benki kuu pia imearifu kuwa Taasisi nyingine ambazo zinatoa huduma za fedha tofauti na ambazo zimesajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania siyo halali na hivyo Umma unashauriwa kujiepusha nazo.
