Taasisi ya CHAGEI kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeongoza zoezi la usafi wa fukwe za Ziwa Nyasa katika eneo la Mbamba Bay ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani ambayo hufikia kilele chake kila tarehe 5 Juni.
Zoezi hilo lililohusisha utoaji wa vifaa vya kuhifadhia taka na kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii, limebeba dhamira ya kulinda mazingira na kurithisha kizazi kijacho mazingira safi na salama.
Wananchi wa Mbamba Bay, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Limbo, wavuvi pamoja na maafisa wa serikali walishiriki kwa pamoja katika kusafisha fukwe hizo na kuonyesha mshikamano wa pamoja katika kulinda hazina ya asili ya Ziwa Nyasa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Furaha Wanjarwa alilipongeza zoezi hilo akibainisha kuwa halmashauri yake imejipanga kuendeleza shughuli za usafi mara kwa mara katika maeneo ya fukwe ili kuunga mkono juhudi za kutunza mazingira. Aidha, alitoa wito kwa wananchi na wavuvi kufanya usafi wa mazingira kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Wilaya hiyo, Denis William, alihimiza jamii kutambua kuwa usafi wa mazingira si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi. Alisisitiza kuwa usafi unapaswa kufanyika kila mahali, si tu katika maeneo ya fukwe, na viongozi wapo tayari kushirikiana na jamii wakati wowote kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi (BMU) wa Mbamba Bay, Adrea Ligola, alisema kuwa ujio wa CHAGEI katika eneo hilo umeongeza hamasa kwa wavuvi kuendelea kushiriki katika shughuli za usafi.

Alieleza kuwa wamejiwekea utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kama sehemu ya kuenzi mazingira yanayowazunguka.
Mwalimu Beatrice Milinga wa Shule ya Sekondari Limbo, ambaye ni mlezi wa wanafunzi marafiki wa CHAGEI, alisema kuwa shule hiyo ina mpango wa kuanzisha rasmi klabu ya CHAGEI kwa lengo la kuendeleza elimu ya mazingira kwa wanafunzi.
Alisema kuwa wanafunzi hao watakuwa mabalozi wa CHAGEI na watasaidia katika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na upandaji miti.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CHAGEI, David Haule, alieleza kuwa taasisi hiyo inalenga kushughulikia kwa pamoja masuala ya usafi wa mazingira na kijinsia.
Alisema kuwa usafi wa Ziwa Nyasa ni sehemu ya mpango kazi wa taasisi yao na zoezi hilo litaendelea kuwa endelevu. Pia alitoa pongezi kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa kwa ushirikiano waliouonesha, akiahidi kuwa ushirikiano huo utaendelezwa kila mwaka.
Kupitia zoezi hili, CHAGEI na wadau wake wameonyesha kuwa mabadiliko ya kweli katika utunzaji wa mazingira yanawezekana pale jamii inaposhirikishwa moja kwa moja na kupewa nafasi ya kuchukua hatua.