Haiti yaunda baraza la mpito

Haiti  imeunda rasmi Baraza tawala la mpito lililopewa jukumu la kujaza pengo la uongozi katika taifa hilo na kurejesha hali ya utulivu kufuatia ghasia zilizosababishwa na magenge ya kihalifu.

Amri ya kuundwa kwa baraza hilo imetangazwa siku ya jana kupitia gazeti rasmi la “Le Moniteur”ikiwa ni mwezi mmoja baada ya Waziri Mkuu Ariel Henry kusema kuwa atajiuzulu kutokana na wimbi la mashambulizi ya magenge yenye silaha katika mji mkuu wa Port-au-Prince.

Tangazo hilo, ambalo  limecheleweshwa kwa wiki kadhaa na mizozo ya kisiasa, ni hatua ya matumaini katika juhudi za kupelekwa kikosi cha polisi wa kimataifa kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa, kikiongozwa na Kenya.

Amri hiyo inalipa baraza hilo jukumu la “haraka” kuteua waziri mkuu mpya na serikali “ikijumuisha” mirengo mbalimbali ya kisiasa na kuundwa kwa baraza hilo linaloungwa mkono na Marekani pia ni hatua ya kwanza kuelekea kufanyika uchaguzi wa rais ifikapo mwaka 2026.

Hata hivyo, maswali bado yamesalia ikiwa serikali ya mpito, iliyopewa jina la Baraza la Mpito la Rais, itaweza kuwa na nguvu dhidi ya magenge ya kihalifu yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu Port-au-Prince.

Nchi hiyo haijafanya uchaguzi tangu 2016 na imekuwa bila rais tangu Jovenel Moise alipouawa mwaka 2021, miongoni mwa atahri zilizosababaishwa na magenge ya kihalifu ni pamoja na kuachiliwa kwa Wafungwa wapatao 4,000  baada ya kuvamia na kushambulia magereza makubwa mawili,kushambulia  vituo vya polisi na uwanja wa ndege.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, lilionya kuwa njaa na utapiamlo vinaendelea kushuhudiwa nchini katika nchi hiyo ambayo licha ya kukabiliwa na zahama za magenge ya kihalifu bado inaendelea kuhangaishwa na  athari za tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2010 lililosababisha vifo vya maelfu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *