FISI MWENYE SHANGA AIBUA MAPYA ITILIMA, DC ATAKA MMILIKI AJISALIMISHE

Na Saada Almasi-Simiyu.

Hali ya sintofahamu imeibuka katika Kijiji cha Kimali kilichopo Kata ya Nyamalapa Wilayani Itilima Mkoani Simiyu, baada ya Fisi mmoja aliyeuawa na vikosi vya Askari wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA),TANAPA pamoja na jeshi la Polisi kubainika kuwa na alama ya jina katika paja lake la kushoto pamoja na hirizi na shanga shingoni mwake ishara ya kwamba alikuwa akimilikiwa na Mtu binafsi

Akiongea na Wananchi katika Kijiji cha Mwamigagani Kata ya Mwalushu Wilayani humo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Anna Gidarya amewataka Wananchi wote wanaomiliki nyara hizo za Serikali bila kibali kutoka mamlaka husika kusalimisha haraka iwezekanavyo kabla ya hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.

Amesema, “unawezaje kumiliki fisi, kwa matumizi gani na umepewa kibali na nani? wewe ambaye unajua unammiliki jisalimishe haraka kabla hatujakufikia mnawafanya watu waishi kwa wasiwasi tunapambana kuleta amani kumbe yupo mtu ambaye anajua kinachoendelea tukikukamata hatua kali zitachukuliwa dhidi yako.”

Desemba 20,2024 baada ya tukio la fisi kuuwa Watoto katika makazi yao Wilayani Itilima na kuweka idadi ya watu 9 kuuawa Wilayani Maswa na Itilima kuanzia mwezi Novemba, Mkuu wa Mkoa huo, Kenani Kihongosi aliunda timu maalumu iliyohusisha vyombo vya kiusalama kwa lengo la kuwasaka na kuwadhibiti Wanyama hao, iliyoanza kazi rasmi Januari 25, 2025 kwa ufanisi.

Tangu kuanza kwa oparesheni timu hiyo imefanikiwa kuua fisi 16 kwa nyakati tofauti na kurejesha matumaini ya kuwepo kwa hali ya usalama mkoani humo.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, amewataka Wananchi kuendelea na majukumu yao kama kawaida huku akikemea vikali imani za kishirikina miongoni mwao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *