DORIA MAALUM YANASA WATUHUMIWA 66, VIPANDE 68 VYA MENO YA TEMBO

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Wazi wa Maliasili na Utalii Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema, katika doria maalum zilizofanyika zimewezesha kukamatwa jumla ya watuhumiwa 66, vipande 68 vya meno ya tembo, magamba 546 ya kakakuona, kobe 132, kenge 13 na aina mbalimbali ya mijusi 213 iliyokuwa ikisafirishwa kwenda nje ya nchi, bunduki mbili (2) na risasi 18 zilizokuwa zikitumika kwenye matukio ya ujangili.

Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo leo Mei 19,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 .

“Katika kukabiliana na ujangili nchini, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kupambana na Ujangili wa mwaka 2023-2033 kwa kuratibu doria maalum zinazoongozwa na taarifa fiche kupitia Kikosi Kazi Taifa Dhidi ya Ujangili kwenye mifumo Ikolojia mbalimbali nchini na maeneo ya mpakani kati ya Tanzania, Kenya na Zambia,”amesema. 

Aidha, amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wa Uhifadhi imefanikiwa kuingiza mada zinazohusiana na masuala ya biashara haramu ya nyara kwenye mitaala inayotumika kufundishia vyuo vya Jeshi la Polisi  nchini. 

“Utaratibu huu umeimarisha uwezo wa Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi katika utambuzi wa nyara na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu katika usafirishaji haramu wa nyara na mbinu za kukabiliana na vitendo hivyo,”amesema. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *