Watoto wawili wa familia moja, Esta Baraka aliyekuwa akisoma darasa la awali na Derick Baraka aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya Msingi Shunu wamefariki dunia baada ya kuzama katika dimbwi la maji walipokuwa wakiogolea katika Mtaa wa Hongwa kata ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa huo Gabriel Mwita ameiambia Jambo Fm kuwa tukio hilo limetokea leo April 23,2024 saa nne asubuhi wakati watoto hao wakiogelea katika dimbwi hilo lililopo kwenye kiwanja kinachomilikiwa na shule ya msingi Dan Viva.
Nao Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamelalamikia uwepo wa madimbwi yenye maji yaliyotuama katika Mtaa wao na kutoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kuwatuma watoto kazi katika muda wa masomo badala ya kwenda shule.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa jeshi la Zima moto na uokoaji wilaya ya Kahama Stanley Luhwago ametoa wito kwa wananchi wa kufunika na kufukia mashimo na visima vyote ambayo havitumiki katika makazi yao na kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la Zima moto na Uokoaji pindi matukio yanayohitaji huduma ya uokoaji yanapojitokeza.