DC MWENDA AKAGUA UJENZI SEKONDARI YA AMALI KITUKUTU

Na Saulo Stephen – Singida. 

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Yusuph Mwenda, ametembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari, Amali Kitukutu, iliyopo katika Kijiji cha Kitukutu, Kata ya Ulemo ikiwa ni mradi mkubwa wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.6 unatekelezwa na Serikali kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Katika ziara hiyo, DC Mwenda aliwataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka ili kukamilisha kazi zilizobaki ndani ya muda mfupi huku akisisitiza kuwa ujenzi huo ni wa muhimu kwa maendeleo ya elimu katika eneo hilo na unapaswa kukamilika haraka ili wanafunzi waanze kunufaika.

“Tupo nyuma ya mradi huu kwa nguvu zote. Hakikisheni ndani ya wiki mbili zijazo mmemaliza maeneo yote yaliyosalia kama karakana, ili kazi ikamilike na watoto waanze masomo mapema,” alisema DC Mwenda kwa msisitizo.

Mradi wa ujenzi wa shule hiyo unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Jengo la Utawala, Madarasa 8, Maabara za Kemia na Baiolojia, Maktaba, Chumba cha TEHAMA, Matundu 11 ya vyoo.

Pia, Kichomea taka, Tanki la maji la ardhini, Mabweni 4, Bwalo la chakula, Karakana za Ufundi Umeme na Ufundi Uashi, Nyumba ya mwalimu mmoja, Viwanja vya michezo: mpira wa miguu, wavu (volleyball), mikono na pete (netball).

Mradi huu unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa elimu bora na stadi za maisha kwa vijana wa Kitanzania zaidi ya 320.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *