CHANGAMOTO YA MAGUGU MAJI ZIWA VICTORIA KUPATIWA UFUMBUZI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika Ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuhakikisha  shughuli za kijamii zinaendelea katika maeneo hayo.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Mei 19, 2024, wakati alipokagua udhibiti wa gugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi maarufu kama daraja la JP. Magufuli.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji ndani ya Ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea,” alisema Waziri Mkuu.

Amesema kuwa magugumaji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika Ziwa Victoria, na hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketeza gugumaji kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa pia ametoa shukrani kwa wananchi wa maeneo hayo, wakiwemo wavuvi, kwa kujitoa kwao kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugumaji hayo. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea bila vikwazo

Akitoa taarifa kuhusu zoezi la utoaji magugumaji katika eneo hilo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amebainisha kuwa juhudi zinaendelea katika eneo la Kigongo-Busisi kushughulikia gugumaji la asili aina ya Lutende huku akisema jumla ya ekari 65 zimeshughulikiwa katika kipindi cha wiki moja, na lengo ni kumaliza ekari zote kabla ya Juni 10 mwaka huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tafiti ya Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Menan Jangu, amesisitiza kuwa Ziwa Victoria lina gugumaji lililogawanyika katika aina tatu: Salvinia Molesta (gugumaji jipya), Water Hyacinth, na Gugumaji la asili aina ya Lutende.

Kuhusu hatua za muda mfupi, Dk. Jangu alieleza kuwa zoezi la uopoaji lilianzia katika eneo la Kigongo-Busisi, ambapo tani 840 za gugumaji zimeondolewa kati ya Februari na Mei 18 mwaka huu. Aliongeza kuwa gugumaji aina ya Water Hyacinth limekwishadhibitiwa na Serikali kupitia Bonde la maji la Ziwa Victoria.

Aidha, katika utekelezaji wa mkakati huo, mchakato wa manunuzi wa mitambo miwili maalumu ya kuopoa magugumaji umefanikiwa, na mtambo mkubwa wa kuondoa gugumaji aina ya Lutende unatarajiwa kufika kabla ya mwisho wa mwezi Julai 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *