Mkuu wa mkoa wa Tabora, Paul Chacha amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa huo kumsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Tabora, Mayala Mburi kwa tuhuma za matumizi ya Lugha zisizofaa kwa Wateja.
RC Chacha ametoa maelekezo hayo akiwa Ofisi ya Wakala huyo, baada ya yeye pamoja na Watumishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kupiga simu kwa nyakati tofauti majira ya usiku kwa lengo la kuhitaji huduma ya Mafuta katika kituo cha Serikali wakiwa safarini kuelekea Mkoa wa Geita na badala yake meneja huyo aliwajibu isivyo huku akidai anapata starehe kwa wakati huo.
“Aliwasiliana yeye mwenyewe na watumishi sita kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wanaenda kwenye tukio kubwa Geita akawambia mkifika mida ya saa mbili au saa tatu (usiku) mtahudumiwa na bahati mbaya watumishi hao wamefika majira ya saa tatu usiku.

“Wakapiga simu kuanzia saa tatu mbaka saa nne simu haijapokelewa badala yake ikaja kupokelewa majira ya saa nne na nusu aliwatukana matuzi ya nguoni huyu bwana anawaambia ninyi ni nani mnanipigia simu usiku huu simu mimi nipo kwenye starehe zangu,” alisema Chacha.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa Mkoa, Meneja huyo aliendelea kuwajibu kwenye simu akisema “nani aliyekupa Mamlaka ya kunipigia simu mimi Meneja wa Kituo (GPSA) usiku huu niamke niache starehe zangu nije kukuhudumia.”
Aidha, katika hatua nyingine Chacha ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi wawili wa Wakala wa Barabara Nchini Mkoa wa Tabora (TANROADS), Meshack Deogrtius na Godfrey Gration wasimamizi wa kituo cha mizani cha Tuli.
Watumishi hao wanatuhumiwa kupokea Rushwa ambapo imetajwa kuwa siku ya ijumaa ya Tarehe 14 Februari 2025, walikamata gari ambalo mzigo ulikuwa umezidi lakini baadae waliliachia gari hilo, baada ya kupokea Rushwa kutoka kwa Mmiliki.