Mwanamke Mmoja aliyefahamika kwa jina la Justina Poul (34), Mkazi wa Mtaa wa 14 Kambarage Kata ya Buhalala Halmashauri ya Mji wa Geita, amenusurika kuuwawa na mtu anayedhaniwa kuwa ni mume wake, baada ya kumjeruhi shingoni na mikononi kwa kutumia kitu chenye ncha kalina baadaye kujinyonga.
Wakizungumza na Jambo FM, baadhi ya mashuhuda wamesema tukio hilo limetokea Novemba 22, 2023, ambapo waliamka asubuhi na kukuta damu nje ya chumba walichokuwa wakiishi wawili hao, na baada ya kubisha hodi hakuna aliyeitikia na walipoingia ndani walikuta mwanaume huyo amejinyonga huku mwanamke akiwa chini na walipomkagua wakagundua hajafariki ndipo walipomkimbiza hospitali kuokoa maisha yake.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita Dkt. Mfaume Salum amekiri kumpokea mwanamke huyo na kusema baada ya kumfanyia uchunguzi wamebaini amejeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wake na kitu chenye ncha kali kwenye shingo, mikononi pamoja na mabegani na sasa anaendelea vizuri. Jambo Fm inaendelea na juhudi za kulitafuta jeshi la polisi mkoa wa Geita ili kupata taarifa zaidi juu ya tukio hilo.