Staa wa TikTok kutoka nchini Indonesia, Lina Mukherjee amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kutokana na video aliyo-post inayomuonesha akisema neno linalotumiwa na Waislamu la ‘Bismillah’ kabla ya kula nyama ya nguruwe, jambo ambalo limelaaniwa vikali nchini humo.
Neno hilo hutumiwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wanapoanza Dua, kula au shughuli mbalimbali wakimaanisha wanaanza ‘Kwa jina la Mungu/Allah’, ambapo katika video hiyo, Lina alionekana akisema Bismillah kabla ya kula chakula kisha akaanza kula nyama ya nguruwe ambayo kwa mafundisho ya Dini hiyo, ni kitu kilichopigwa marufuku (Haram).
Lina aliripotiwa na Jirani yake na video hiyo imekusanya mamilioni ya Watu waliotazama mtandaoni, amepatikana na hatia ya ‘kueneza habari zinazolenga kuchochea chuki dhidi ya Watu wa Dini na makundi maalum’ katika Mahakama moja iliyopo Mji wa Palembang nchini Indonesia.
Mukherjee ambaye anasema yeye ni Muumini wa Dini ya Kiislamu pia amepigwa faini ya Rupiah milioni 250 (Tsh Mil 40), Indonesia ndio Taifa kubwa zaidi lenye Waislamu wengi duniani na lina sheria kali dhidi ya makosa ya kukiuka mafundisho ya Dini hiyo.