TANZANIA IMETENGA BILIONI 476 KUINUA SEKTA YA MIFUGO – DKT. KIJAJI

Na Saada Almasi – Simiyu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga zaidi ya bilioni 476 katika sekta ya mifugo kwa lengo la kuiimarisha na kuiinua sekta hiyo ambayo inachangia zaidi ya asilimia 6.2 katika pato la Taifa

Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt Emmanuel Nchimbi alipokuwa mkoani Simiyu katika Kongamano la wafugaji lililofanyika katika kata ya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani humo.

Hili linakuja ikiwa ni siku moja kabla ya uzinduzi wa chanjo ya mifugo unaotarajiwa kufanywa na raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia Dkt Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa bajeti iliyokuwepo mwaka 2021/2022 ilikuwa bilioni 66 hivyo ongezeko hilo linaonyesha nia ya dhati ya serikali katika kuwaunga mkono wafugaji nchini

“kiasi ambacho sekta ya mifugo inachangia ni asilimia zaidi ya 6.2 na hii inaonyesha ukubwa wa sekta hii katika kuijenga nchi yetu na ndiyo maana ndani ya miaka minne mmeona ongezeko kubwa katika bajeti ya sekta ya mifugo,” amesema Nchimbi.

Aidha ameongeza kuwa serikali inatambua kuwa mifugo ni sekta muhimu ya kuzalisha ajira na kipato kwa ufugaji hivyo itaendelea kiimarisha upatikanaji wa maeneo ya ufugaji wa kisasa,kuboresha miundombinu katika maeneo hayo kama upatikanaji wa maji na umeme ili waweze kufanya shughuli za uchakataji wa mazao ya mifugo.

“tumedhamiria kuongeza umilikishwaji wa maeneo ya ufugaji kutoka hekta milioni 3 hadi hekta milioni 6 na maeneo hayo yataboreshewa miundombinu muhimu yote,pia tutakarabati mabwawa na kuchimba visima virefu hadi kufikia 285,kuongeza maafisa ugani,kurahisisha upatikanaji wa mbegu na kuimarisha utoaji wa elimu juu ya ufugaji wa kisasa ili mazao ya mifugo Yazidi kuongezeka,” ameongeza Nchimbi.

Awali akizungumza na wafugaji katika kongamano hilo waziri wa Mifugo na Uvuvi Ashatu Kijaji amesema kuwa wizara itaendelea kushirikiana na wadau wake kujadili changamoto wanazozipitia na kuona namna ya kuzigeuza kuwa fursa ili ziwanufaishe.

Ameongeza kuwa hadi sasa serikali imekwisha fanya jitihada katika kuongeza uwekezaji katika viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo ili kuleta chachu katika ufugaji hivyo ni wajibu wa kila mfugaji kuhakikisha anatoa malighafi za kutosha ili ziweze kulisha viwanda hivyo.

“Ndani ya mwezi huu wa kumi mkoani Shinyanga tunakwenda kufungua kiwanda kikubwa cha kuchakata maziwa cha Jambo ambacho kitahitaji kila baada ya saa moja kupatikane maziwa lita 5000 fursa ambayo imeletwa na serikali hivyo ni wajibu wa kila mfugaji kuhakikisha malighafi za kiwanda hicho zinapatikana,“ amesema Waziri Ashatu.

Aidha amewataka wafugaji hao kuzingatia namna sahihi ya ufugaji wa kisasa ,tudhibiti magonjwa kwa mifugo na kusema kuwa wizara tayari imekwisha wapatia eneo jijini Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya chama cha wafugaji ili waendelee kuleta mchango katika pato la Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *