Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro ametoa siku saba kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexius Kagunze kushughulikia hoja 28 zilizosalia kati ya hoja 31 zilizoibuliwa katika ripoti iliyopita ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka mchakato wa ufungaji wa hoja hizo utekelezwe kabla ya mwaka wa fedha ujao.
Wakili Mtatiro amebainisha hayo kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha leo Juni 12, 2025 wakati akihutubia Baraza Maalum la Madiwani, lililoketi ili kupitia taarifa ya CAG, iliyokaguliwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024.

Akiwasilisha majibu ya hoja za CAG, Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, CPA. Peter Tarimo amesema hoja 31 ziliibuliwa, ambapo 3 tayari zimetekelezwa kikamilifu na kufungwa, huku hoja 28 zikiendelea kufanyiwa kazi na Menejimenti kwa kuwasilisha majibu na vielelezo kwa Mkaguzi Mkuu wa Nje kwa ajili ya uhakiki na wamepata Hati Safi.
“Mwenyekiti kwa kipindi cha kuishia terehe 30 Juni 2024 Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ilifunga hesabu zake na kuziwasilisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,na kutokana na Hesabu hizo Halmashauri imepata Hati Safi,” amesema CPA Tarimo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Ibrahimu Makana ameipongeza Manispaa hiyo kwa kupata Hati Safi, huku akisisitiza kuwa katika hoja 28 ambazo zimesalia vielelezo vyake vipatikane na kuhakikiwa ili hoja hizo zipate kufungwa.
Naye Mkaguzi wa Nje kutoka ofisi ya mkaguzi ana mdhibiti wa hesabu za serikali katika mkoa wa Shinyanga, CPA Yusuph Mabwe, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata Hati Safi, na kwamba Hati hiyo imetokana na usimamizi madhubutu wa utekelezaji wa shughuli za Halmashauri na Rasilimali za Umma ipasavyo.

Akizungumzia maagizo yaliyotolewa na wakili Mtatiro Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko amesema maelekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi,kwa utafutaji wa vielelezo sababu hoja zote zinajibika, ili ziweze kufungwa huku akiwataka Wakuu wa Idara katika manispaa hiyo kutoa ushirikano katika kupata vielelezo.