Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari Mkoani Mwanza kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kufahamu huduma zinazotolewa na mfuko huo na pamoja na kuimarisha mahusiano.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika hii leo Juni 12,2025 katika ukumbi wa hoteli ya Gold Crest yakishirikisha zaidi ya wanahabari 30 wa mkoa wa Mwanza.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Kaimu Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa, Happness Manyenye amesema mfuko huo umeboresha huduma zake ikiwemo wanachama kujiandikisha na kupata taarifa za mafao yao kidigitali kupitia mfumo wa ‘PSSSF Member Portal’.
Aidha katika hatua nyingine Happiness ameongeza kwa kusema kua kwa sasa kima cha chini cha Pensheni kimeongezeka mpaka kufukia Shilingi laki moja na nusu Ongezeko ambalo ni sawa na asilimia mbili.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Abdul Njaidi amesema katika kuondokana na utegemezi wa michango ya wanachama mfuko huo umekua ukibuni miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa majengo, viwanda pamoja na miradi mingine jambo ambalo limekua likiwasiaidia kukua kiuchumi pamoja na kuwasaidia kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mahusiano mema baina ya PSSSF na wanahabari na kwamba yataongeza weledi wakati wa kuandika habari na kuelimisha za jamii na watumishi wa umma kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huo.

Naye Jane Kalimasi ambae ni Muuguzi Mstaafu na mnufaika wa mfuko huo ameipongeza PSSSF kwa maboresho mazuri ya mfumo wa uhakiki kwani mstaafu anaweza kupata taarifa zote muhimu kupitia simu ya mkononi bila usumbufu wowote.