WAISLAMU BARIADI WATOA UJUMBE SIKU YA EID EL ADHA

Na Saada Almasi  – Simiyu.

Waamini wa dini ya Kiislamu Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameungana na waislam kote nchini kuadhimisha sikukuu ya Eid el Adha ambayo huadhimishwa kwa kuchinja baada ya ibada ya hija kwa waislamu waliopata uwezo wa kwenda kuhiji mji mtukufu wa Makka

Mjini Bariadi swala ya eid imefanyika katika msikiti mkuu wa BAKWATA ambapo Sheikh Mkuu wa Mkoa huo, Issa Kwezi amewaasa waumini wa dini hiyo kulinda maadili na utu wa kila mtu bila kujali yeye ni nani sambamba na kutumia lugha za staha katika kukosoana kwani kwa kufanya hivyo ni kulinda tunu ya amani ambayo inaongoza Taifa.

“maadili yetu ya nchi yanatutaka tumheshimu kila mtu bila kujali ni nani na viongozi wetu tuwape heshima yao inayostahiki kama kuna namna ya kukosoana tukosoane wa adabu na lugha njema zisiwe lugha za kashfa kwani huyo unayemfikishia ujumbe anaweza asizingatie kwa sababu ya namna ujumbe ulivyofikishwa” amesema Sheikh Kwezi

Awali akitoa hotuba ya swala imamu wa msikiti huo Yabub Saburi Yakub amewataka waamini kutumia milango yao ya fahamu kwa usahihi kufikiria kuona na kuhisi machungu ambayo watu wa nchi zilizopoteza amani kwa vita wanazipitia ili iwe funzo kwao.

” tumieni milango yenu ya fahamu kufikiria,kuona na kusikia,na mioyo yenu kuhisi machungu ambayo wanayapitia wale ambao hawana amani katika nchi zao,huo utakuwa ukumbusho kwamba uilinde na kuitunza amani ya nchi yako ili usifikie huko,” imamu Yakub.

Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ni Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Salum Mwalimu ambaye kwa upande wake amewaasa waislamu kuitikia wito wa kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi huku akiwapa ujumbe watakaosimamia uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu kuwa waadilifu kwa kutenda haki kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

” niwaombe waislamu wa mji huu jitokezeni kwa wingi katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi msiangalie tu kwamba fulani na fulani ndiyo wanafaa mimi sifai hapana,lakini pia kwa watakao pata nafasi kusimamia uchaguzi zingatieni maadili,muwe waadilifu na mtende haki,” amesema Mwalimu.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa mkoa huo Moza Ally amewaomba waislamu kutumia siku ya Eid katika kuambiana mambo mema na kutoruhusu wanasiasa kuwatumia kwa nia mbaya ambayo itavuruga amani iliyopo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *