Katika kijiji cha Mipotopoto, kilicho pembezoni mwa Pori la Akiba la Liparamba Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, hali ya taharuki ilitanda kufuatia kuonekana kwa simba mwenye rangi isiyo ya kawaida mwenye rangi mchanganyiko wa kahawia na nyeupe, ambaye aliingia katika makazi ya binadamu.
Tukio hilo, ambalo sasa limeacha maswali mengi kwa Wanakijiji na Wanasayansi wa wanyamapori, lilianza takribani siku nne zilizopita wakati mwananchi mmoja alinusurika kifo kwa miujiza baada ya kukutana uso kwa uso na mnyama huyo porini alipokuwa akitoka shambani. Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Mipotopoto Said Mahamud, mkazi huyo alifanikiwa kujiokoa kwa kupanda mti na kujificha.

Tahadhari iliongezeka baada ya usiku mmoja baadaye, simba huyo kufanya tukio lisilo la kawaida – alipanda juu ya paa la nyumba moja, akavunja dirisha, na kumchukua mbwa kabla ya kutokomea gizani huku akiwa ameondoka pia na baadhi ya nguo zilizokuwa ndani.
Lakini hali ilizidi kuwa mbaya zaidi usiku uliofuata, ambapo alivamia zizi la mifugo na kuua kondoo watano pamoja na mbuzi mmoja, jambo lililoibua hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Serikali ilichukua hatua kwa kuwatuma askari wa wanyamapori kutoka kituo cha Mbinga waliokuja kufanya ufuatiliaji wa tukio hilo. Hatimaye, simba huyo alidungwa risasi na kuuawa, na ngozi yake kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi.
Inaelezwa kuwa simba huyo alikuwa dume, mwenye umbo kubwa na dalili za kudhoofika kiafya – hali inayodhaniwa kuwa ndiyo iliyopelekea kuvuka mipaka ya hifadhi na kuingia katika makazi ya watu, jambo lisilo la kawaida katika historia ya eneo hilo.

Diwani Mahamud amesema tukio hilo ni la kipekee na halijawahi kushuhudiwa kwa miaka mingi tangu hifadhi hiyo kuwepo. Wananchi wameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua kwa haraka na kuzuia madhara zaidi ambayo yangesababishwa na mnyama huyo.
Simba wenye rangi kama hiyo ni adimu sana duniani, na mara nyingi huonekana katika maeneo maalum tu – na Pori la Akiba la Liparamba likiwa mojawapo ya sehemu hizo nadra. Kifo cha mnyama huyo kimeacha hisia mseto, kati ya huzuni kwa kupotea kwa kiumbe wa kipekee na faraja kwa usalama wa wanakijiji.