UJENZI WA DARAJA MABATINI: RC MTANDA AMPA MAAGIZO MKANDARASI

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda amemtaka mkandarasi anaetekeleza ujenzi wa daraja la Mabatini jijini Mwanza kukamilisha daraja hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja aliopewa, ili liweze kuanza kutumika na wananchi.

Mtanda ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo unaotekelezwa na kampuni ya Nyanza Roads Work ambapo amesema hatovumilia ucheleweshaji endapo halitakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

“Tayari nimesikia mkandarasi umeshalipwa na Serikali fedha za utangulizi Tshs. Milioni 600 na makubaliano ya mkataba ni muda wa mwaka mmoja hivyo nataka kuona Novemba mwaka huu kazi hii iwe imekamilika’, amesema Mtanda.

Katika hatua nyingine Mtanda pia amesema daraja hilo ni daraja muhimu sana katika mkoa wa Mwanza kwani linaunganisha barabara kuu ya kwenda mikoa ya Mara na Simiyu hivyo endapo litakamilika kwa wakati litarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani.

Aidha pia Mtanda pia amewataka Wakala ya Barabara TANROADS kusimamia kwa karibu kazi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambroce amesema ujenzi wa daraja hilo utagharimu  zaidi ya Tshs bilioni 6.3 na wamejipanga kuusimamia kwa ukaribu ili mradi huo uweze kukamilika katika muda waliokubaliana .

Nae kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Mwanza MWAUWASA mhandisi Nelly Msuya amesema shughuli za kubomoa daraja lililokwepo katika eneo uliharibu miundombinu ya maji iliyokua imepita katika eneo hilo ila kwa sasa tayari wameboresha miundombinu yote na wananchi wanapata huduma ya maji kama kawaida.

“Ukarabati huu umeigharimu miundombinu yetu kuhamishika kazi ambayo imesababisha kuwepo na ukosefu wa maji siku za nyuma lakini hivi sasa hall ya upatikanaji wa huduma ya maji imerejea kama kawaida kasoro maeneo machache ya pembezoni mwa Jiji kutokana na kazi ya kutandaza mabomba inaendelea’, Nelly Msuya, Meneja MWAUWASA mkoa wa Mwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *