Na Frank Aman – Geita.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu wawili Ismail John (25), anayejihusisha na Shughuli za Kilimo na Bosco John (28), Mwendesha Boda boda kwa tuhuma ya wakijifanya Maafisa wa Polisi baada ya kuwalaghai wananchi kisha kuwaibia pesa na mali zao na kukimbia nazo.
Watuhumiwa hao wamekamatwa Aprili 7, 2025 saa 2 usiku katika Mtaa wa Samina uliopo Kata ya Mtakuja wilayani Geita baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za siri juu ya uwepo wa watu wawili ambao wamekuwa wakijifanya Maafisa wa Polisi baada ya kuwalaghai wananchi kisha kuwaibia pesa na mali zao kisha kukimbia.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi liliweka mtego na uliofanikisha kukamatwa watuhumiwa hao wakiwa katika mtaa huo wakifanya vitendo vya kihalifu huku wakiwa wamepora kiasi cha Sh25,000 kwa mwananchi mmoja (ambaye jina linahifadhiwa).
“Watuhumiwa hawa wamehojiwa kwa mujibu wa sheria na wamekiri kujihusisha na vitendo vya kihalifu baada ya kujifanya Maafisa wa Jeshi la Polisi katika maneno mbalimbali ya Mkoa wa Geita,” amesema.
RPC Jongo amesema kuwa taratibu za kisheria zikikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili, ambapo pia amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita litatoa onyo kwa mtu yeyote ama kikundi kujifanya maafisa ama watumishi wa serikali kwa lengo lolote lile waache mara moja na atayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.