MFUMUKO WA BEI 2024 UMEPUNGUA KWA WASTANI WA ASILIMIA 3.8 – MAJALIWA

Mfumuko wa bei kwa mwaka 2024 umepungua hadi kufikia wastani wa asilimia 3.1 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Bungeni jijini Dodoma hii leo Aprili 9, 2025 na kuongeza kuwa kiwango hicho kipo ndani ya lengo la nchi na Jumuiya za kikanda la wigo wa asilimia 3.0 hadi 5.0 katika muda wa kati.

Amesema, kupungua kwa mfumuko wa bei kulitokana na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na bajeti; uwepo wa utoshelevu wa chakula nchini na uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi iliyorahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka maeneo ya uzalishaji hadi kwenye masoko.

“Mwenendo wa viashiria vya uchumi na bajeti katika mwaka 2024/2025 umeendelea kuwa wa kuridhisha. Katika mwaka 2024, Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.1 mwaka 2023,” amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa, ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme; uimarishaji wa huduma za jamii; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi; kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji; na kuimarika kwa sekta ya uchukuzi.

Aidha, Waziri Mkuu amesema sekta zilizokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji katika kipindi cha marejeo ni pamoja na shughuli za sanaa na burudani asilimia 17.1, fedha na bima asilimia 16.3, na habari na mawasiliano asilimia 14.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *