Na Iddi Banza
Ni nusu karne sasa (miaka 50) imetimia, tangu Dunia iliposhuhudia pambano maarufu zaidi Duniani lililoandika historia kubwa katika bara la afrika na Dunia kwa ujumla, la ‘Rumble in the jungle’ kati ya George Foreman dhidi ya Muhammad Ali kufanyika.
Pambano hilo lililoikutanisha miamba ya masumbwi ya uzito wa juu Duniani, lilikuwa la raundi 15 na lilipigwa siku kama ya leo (Oktoba 30) mwaka 1974 kwenye uwanja wa soka wa Stade Tata Raphael mjini Kinshasa, DR Congo (zamani Zaire), miamba hiyo ilikuwa ikiwania ubingwa usio na kifani ‘Undisputed Championship’ katika zama za mikanda miwili (WBA na WBC).
Foreman alipanda ulingoni siku hiyo kulitetea taji lake la ‘Undisputed’ alilolitwaa Januari 1973 nchini Jamaica kwenye uwanja wa taifa wa Kingston kwa kumchapa TKO raundi ya pili mkali Smokin’ Joe, Joe Frazier. Foreman alikwenda akiwa hajapoteza pambano lolote, huku Ali alikuwa akienda kuisaka ‘Undisputed’ yake ya tatu, baada ya kushinda mwaka 1964 na 1967.
Mwisho wa pambano mbele ya wahudhuriaji 60,000 Ali aliyekuwa na umri wa miaka 32 alishinda kwa KO raundi ya nane na akawa ‘Undisputed Champion’ kwa mar aya tatu katika uzito wa juu na Foreman aliyekuwa na umri wa miaka 25 akapoteza pambano lake la kwanza baada ya kucheza mapambano 40 bila kupoteza.
KWANINI LILIPIGWA DRC?
Muhammad Ali na George Foreman walimwambia Promota Don King wanahitaji dola za Marekani Milioni 5 ili wacheze pambano hilo, kwa kuwa Don King hakuwa na kiasi hicho cha pesa na hakuwa amekaribishwa kufanya pambano la hadhi hii nchini Marekani ndipo alipoamua kutafuta taifa la nje ya Marekani kuandaa na kudhamini tukio hilo.
Fred Weymar aliyekuwa mshauri wa kimarekani wa mtawala wa taifa la Zaire (DRC) Bwana. Mobutu Sese Seko, alimshawishi Mobutu kwamba kufanya tukio lenye hadhi kama hiyo kutauimarisha utawala wake katika taifa la DRC ndipo Mobutu alikubali na hata Muammar Gaddafi wa Libya alishiriki katika tukio kwa kuwalipa mabondia.
Na kilichobaki ni historia inayoendelea kukumbukwa vizazi kwa vizazi.