Mahakama ya Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa uboreshaji wa mahakama za mwanzo ambazo zilikuwa katika hali chakavu katika halimashuri ya manispaa ya Shinyanga, Kahama na Geita mradi ambao utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 3.6 huku lengo la maboresho hayo ikielezwa kuwa ni kuimarisha utendaji kazi wa muhimili huo.
Akizungumza katika kikao cha makabidhiano ya mradi huo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali amesema mradi huo umekuja kwa muda muafaka kwani kuna uhaba wa majengo ya mahakama za mwanzo na wilaya katika mkoa wa Shinyanga huku akimtaka mkandarasi mshauri kutimiza majukumu yake kwa weledi ili kuzuia ubadhilifu katika mradi huo.
Naye Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Amon Germin amesema kwa mujibu wa makubaliano na muhimili huo anatakiwa kutekeleza mradi huo katika kipindi cha miezi sita pekee huku akiahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa ubora kulingana na fedha husika iliyotumika kugharimia mradi huo.
Aidha Mkandarasi Mshauri katika mradi huo Charles Rwakanadi ameahidi kumsimamia mkandarasi anayejenga majengo hayo ili aweze kutekeleza mradi huo kwa wakati na weledi.