
Baadhi ya Wakazi wa mtaa wa Mbugani na Msalala Road katika Kata ya Kalangalala Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita wamelalamikia changamoto ya wananchi kukusanya taka na kuzichoma moto katika makazi yao badala ya kuzipeleka kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na serikali hali ambayo imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira.
Wamebainisha hayo wakati wakizungumza na Jambo FM ambapo wamesema licha ya serikali kutenga maeno maalum ya kuhifadhia taka lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakichoma taka hizo na kusababisha moshi na harufu mbaya kwenye maeneo ya makazi ya watu pamoja na maeneo ya biashara zao.
Aidha wamesema watu wengi wamekuwa wakifanya vitendo hivyo bila kujua Sheria hususani zinazohusu Mazingira pamoja na kutokujua madhara yanayoweza kujitokeza juu ya uchomaji taka katika maeneo ya wananchi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Msalala Road Sostenes Kalist amekiri uwepo wa changamoto hiyo huku akisema kuwa wananchi wana elimu ya usafi wa mazingira na wanaelewa kuwa kuchoma taka kwenye makazi ya watu ni kinyume na utaratibu lakini wamekuwa wakivunja utaratibu huo kwa kukusudia hivyo amewataka kufuata utaratibu uliowekwa na halmashauri.
Akizungumza kwa njia ya simu na Jambo Fm, Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita Edward Chacha amesema Halmashauri ya Mji hairuhusu kuchoma taka maeneo ya majini na kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.


