Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Wazazi Waaswa Ulinzi wa Watoto,Uwajibikaji ni Tatizo

Na William Bundala,Kahama

Wazazi na walezi katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa  kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wanaowapa mimba za utotoni na kuwakatisha masomo yao.

Rai hiyo imetolewa Juni 16,2024 na Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Sindano William ambaye alikuwa ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.

“Wazazi na walezi mnapaswa kuwalinda watoto walio shuleni dhidi ya vitendo vyovyote vile vinavyolenga kuwakatisha masomo,kuwalinda dhidi ya ajira mbaya na hatari,kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa,kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto na kuwashirikisha kikamilifu katika utekelezaji wa sheria za mtoto pia nayaomba mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya watoto,taasisi za dini kwa kushirikiana na serikali kuzidi kujikita  kutoa elimu yenye maadili na weledi ili kumjenga mtoto kifikra ili kupata jamii yenye maadili”amesema William

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya watoto wa wilaya ya Kahama,Mtoto Simon Emmanuel amesema wazazi na walezi wengi wamekosa uwajibikaji kwa watoto wao katika maelezi na matunzo na kupitia risala hiyo ameiomba serikali kuwawajibisha wazazi ambao wamekuwa wakikwepa kutimiza wajibu wao katika malezi ya watoto.

“Bado zipo changamoto ambazo zinatukabili kama vile wazazi kutotimiza wajibu wao,watoto wenye ulemavu kufichwa wasipate elimu,kutupwa majalalani,kupigwa na kunyanyaswa,sisi watoto wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama tunaiomba serikali,mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii yote iyaone haya yote na kuyatilia mkazo kwa nguvu zote aidha wale wote ambao hawatatekeleza haki zetu wawajibishwe kwa mujibu wa sheria”amesema Mtoto Emmanuel

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na walezi wilayani humo wamewataka wazazi na walezi kutokuwa wagumu katika kufanikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu watoto wao ili kuwaepusha kuingia ktika vishawishi vinavyoweza kuwapelekea  kukatisha masomo kwa kupata mimba za utotoni  na kuwaasa kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo viovu.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika hufanyika kila mwaka Juni 16 na mwaka huu yamefanyika yakiwa na kauli mbiu isemayo Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili, na Stadi za kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *